Karibu

Karibu kwenye Tovuti ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula NFRA, Dhana ya usalama wa chakula nchini ni dhana muhimu ambayo imekuwepo tangu enzi za ukoloni ambapo kufuatia majanga mbalimbali kama vile ukame, mafuriko, nk. Serikali iliwajibika kuchukua hatua madhubuti za kuwasaidia wananchi wake ili wasife kwa njaa.

Dhana ya usalama wa chakula nchini ilipewa umuhimu wa kipekee baada ya uhuru wa Tanganyika mwaka 1961 ambapo serikali ilitilia mkazo kilimo cha mazao ya chakula ili kujitosheleza kwa chakula na kuwa na ziada ambayo wananchi walihimizwa kuitunza na kuihifadhi vizuri kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

Sera na kaulimbiu mbalimbali kama vile “Siasa ni Kilimo”, “Kilimo cha Kufa na Kupona”, “Kilimo ni Uti wa Mgongo wa Taifa Letu”, “Kilimo Kwanza” nk. zililenga kuhimiza wananchi kuzalisha mazao kwa wingi ikiwa pamoja na yale ya chakula. Katika kipindi hiki, uzalishaji wa mazao ya nafaka kama vile mahindi, mtama, uwele, mpunga, ngano, ulezi, nk. Ulipewa kipaumbele.

Pia mazao aina ya mikunde ilipewa msukumo mkubwa kwani kwa utamaduni wa mtanzania haya ndiyo mazao yaliyokuwa yanatumika kama chakula. Pamoja na jitihada za Serikali na wananchi wake kujitosheleza kwa chakula, wakati mwingine juhudi hizi zinaathiriwa na majanga kama vile ukame, mafuriko, milipuko ya magonjwa ya mimea, nk.

Hali hii imekuwa ikitishia usalama wa chakula nchini. Ili kukabiliana na athari za majanga yanayojitokeza, Serikali imekuwa na mikakati mbalimbali mojawapo ni kuwa na chombo maalumu kitakachonunua na kuhifadhi chakula ili kitolewe wakati yanapotokea majanga kuwasaidia wananchi wasiathirike kwa njaa. Mkakati huu ulilenga kuwa na Hifadhi ya Chakula ya Taifa ambayo itawezesha serikali kuwapatia wananchi wake chakula wakati wa majanga.

Lengo la Tovuti hii ni kuelezea kwa kifupi historia ya vyombo vilivyoundwa kwa ajili ya Hifadhi ya Taifa ya Chakula nchini Tanzania, mafanikio na changamoto mbalimbali zilizovikabili vyombo hivi muhimu kwa mustakabali wa kupambana na athari za majanga hususan njaa katika taifa letu.

Vyombo hivi vilipelekea kuundwa kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula ambacho kimepewa jukumu hili kubwa na nyeti kwa usalama wa Taifa letu. Ni matumaini yangu kuwa utaelewa kwa undani historia ya Wakala, ulipotoka, mafanikio, na changamoto inazokabiliana nazo.

Milton M. Lupa

Afisa Mtendaji Mkuu