Wakala unatoa huduma mbalimbali kwa wadau kwa kuzingatia mahitaji ya wakati. Huduma hizo hutolewa kwa gharama nafuu kuwezesha wadau kuzingatia uhifadhi bora wa nafaka unaoweza kusaidia kulinda ubora wa nafaka na kupunguza gharama za uendeshaji wa huduma nyingine. Zifuatazo ni baadhi ya Huduma zinazotolewa na Wakala;
i. Ukodishaji wa maghala;
Wakala unakodisha maghala yaliyopo katika Kanda zake kwa ajili ya uhifadhi kwa kuzingatia mahitaji maalumu ya wakodishaji. Fursa ya kukodisha maghala hupatikana wakati maghala hayo yakiwa hayana akiba ya chakula iliyohifadhiwa na Wakala.
ii. Upimaji uzito;
Huduma ya upimaji uzito wa magari ya mizigo hutolewa kwa gharama nafuu kupitia mizani zilizosimikwa katika maeneo ya Chang’ombe (Mbozi road), Kipawa, Makambako, Songea (Ruhuwiko), Songwe (Eneo la Tazara/ Ichenjezya), Sumbawanga (Mazwi), Mpanda, Shinyanga, Dodoma (Kizota) na Arusha (Themi).
iii. Ushauri kuhusu uhifadhi, unyunyiziaji na ufukiziaji wa nafaka katika maghala;
Wakala ina watalaamu waliobobea katika masuala ya uhifadhi wa nafaka. Wataalamu hawa huweza kutumika katika kutoa elimu ya mbinu bora za uhifadhi hususan katika kutibu/kukinga nafaka zilizohifadhiwa katika maghala kwa gharama nafuu.
iv. Ukodishaji wa maturubai;
Wakala hutoa huduma ya kukodisha maturubai maalumu kwa gharama nafuu kwa ajili ya kufunika nafaka.
v. Utoaji wa elimu kuhusu uhifadhi wa nafaka;
Wakala hushiriki katika matukio mbalimbali ya kitaifa na kimataifa. Miongoni mwa matukio hayo ni ushiriki wa maonesho ya Sabasaba, Nanenane, Siku ya Chakula Duniani na mikutano mingine maalumu. Wakati wa matukio hayo Wakala hutoa elimu kuhusu uhifadhi wa nafaka bure ikiwa ni sehemu ya mchango wake katika maendeleo ya jamii hususan sekta ya kilimo.
vi. Ukodishaji wa Ukumbi wa mkutano;
Wakala una Ukumbi wa mikutano katika baadhi ya Ofisi zake. Ukumbi huu unakodishwa kwa gharama nafuu na upo katika Ofisi za Makao Makuu ya Wakala – Kizota, Dodoma. Ukumbi una uwezo wa kuhudumia idadi ya takribani watu 100 kwa kutegemea mpangilio wa ukaaji.