Ununuzi wa Akiba ya Chakula

UNUNUZI WA AKIBA YA CHAKULA

Wakala una jukumu la kununua nafaka kwa ajili ya akiba chakula ya Taifa ili kukabiliana na majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza. Nafaka zinazonunuliwa kwa sasa ni mahindi, mtama na mpunga na hununuliwa kupitia Kanda mbalimbali za Wakala katika maeneo yaliyobainika kuwa na uzalishaji mkubwa nafaka. Wakati wa kutekeleza jukumu la ununuzi wa nafaka, maandalizi ya awali hufanywa kwa kushirikiana na Mikoa pamoja na Halmashauri zitakazo husika katika ununuzi.

Wakala hufanya uhamasishaji kwa wakulima kwa kuwapa elimu kuhusu vigezo vya ubora wa nafaka kupitia watumishi wabobezi katika fani ya ubora. Katika kalenda ya Wakala zoezi la ununuzi huanza msimu wa mavuno mapya kati ya mwezi Juni na Julai. Muda wa kufunga zoezi la ununuzi hutegemea upatikanaji wa nafaka katika masoko mbalimbali yaliyolengwa.

Maandalizi ya Ununuzi wa Nafaka

Kabla ya kuanza ununuzi Wakala hufanya maandalizi yafuatayo:

i. Kubaini mahitaji ya vifaa na vitendea kazi.

ii. Kubaini vituo vya ununuzi pamoja na vikundi/vyama vya wakulima kwa kushirikiana na Uongozi wa Mikoa na Wilaya, na kuingia navyo mikataba.

iii. Kufanya uhamasishaji katika maeneo ya ununuzi ili kuzingatia viwango vya ubora wa nafaka inayonunuliwa. Msisitizo unawekwa kupitia vikao vya ana kwa ana na wadau na kupitia vipindi vya luninga na redio.

iv. Kupeleka vitendea kazi na vifaa vyote muhimu vya ununuzi kwenye vituo vya ununuzi.

v. Kupanga bei ya kununulia nafaka katika Kanda ambazo zitatumika katika vituo vya ununuzi, vikundi vya wakulima au njia nyingine itakayotumika katika ununuzi wa nafaka. Bei hizo huzingatia gharama za uzalishaji alizoingia mkulima.

Njia za ununuzi wa nafaka;

i. Vituo vya Ununuzi,

ii. Vikundi/SACCOS/AMCOS,

iii. Kutumia Mawakala,

iv. Kutumia Zabuni.

Vigezo vya Ubora vinavyozingatiwa kwa sasa katika ununuzi wa mahindi, mtama na mpunga;

KUHIFADHI MAZAO

Baada ya zoezi la kununua kukamilika Wakala huhifadhi chakula kilichonunuliwa katika maghala ili kiweze kutumika pale kinapohitajika. Kwa sasa, NFRA ina jumla ya maghala 34 yenye uwezo wa kuhifadhi jumla ya nafaka zenye ujazo wa Tani 251,000. Maghala hayo yapo kwenye maeneo muhimu ya uzalishaji na usambazaji nchini. Wakala unatekelezamajukumu yafuatayo katika kuhifadhi nafaka;

i. Kuweka nafaka kwenye magunia yenye uzito wa kilo 50 au kilo 90;

ii. Kupanga magunia ya nafaka kwa utaratibu maalum (katika lusu) yakiwa yamepangwa juu ya chanja (pallets) zilizotandazwa juu ya sakafu;

iii. Kufukiza madawa ya kuua wadudu waharibifu

iv. Kuhamisha mazao kutoka kwenye vituo vya ununuzi kwenda kwenye maghala ya kanda

v. Kuendelea kukagua ubora wa nafaka ndani ya maghala wakati wote wa kuhifadhi nafaka na kufukiza madawa pale inapohitajika

vi. Kuhamisha chakula kutoka katika maeneo yenye uzalishaji mkubwa na kuyapeleka katika maeneo yenye upungufu wa chakula kwa lengo la kuimarisha akiba katika maeneo yenye upungufu sambamba na kutoa nafasi kwenye maghala yenye ziada ya chakula.