Masoko

Moja ya vipaumbele vya Wizara ya Kilimo ni kuwahakikishia wakulima masoko ya ndani na nje ya nchi ili kuwezesha kuuza mazao yao. Katika kutekeleza hilo, Wakala unaendelea kuongeza wigo wa masoko ya nafaka kwa kununua mazao zaidi kutoka kwa wakulima ndani ya nchi na kutafuta masoko ya ndani na nje ya nchi.

Masoko ya ndani

Katika kutekeleza jukumu la ununuzi wa nafaka, Wakala hununua nafaka kutoka kwa wakulima kila mwaka hivyo kuwa soko linalotegemewa kwa kiasi kikubwa na wakulima nchini katika kuuza mazao yao. Wakala imekuwa ikifanya kazi kwa ukaribu na wakulima kupitia vikundi, vyama vya ushirika na wadau wengine. Pamoja na kutoa sehemu ya akiba ya chakula kuhudumia mahitaji ya dharura, sehemu kubwa ya akiba inayohifadhiwa hutafutiwa soko na kuuzwa kwa wadau mbalimbali wakiwamo sekta binafsi inayojumuisha wasagishaji na wafanyabiashara wengine, Taasisi mbalimbali na mashule. Mauzo haya huwezesha Wakala kupata fedha za kununua nafaka zaidi kutoka kwa wakulima nchini.

Masoko ya nje

Ili kufikia azma ya kuongeza wigo wa masoko, Wakala umekuwa ukifanya jitihada za kutafuta masoko mbalimbali ya nje ya nchi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wakala umeendelea kupokea maombi na kuuza nafaka nje kwa kutegemea upatikanaji wa masoko na akiba ya chakula cha kutosha iliyohifadhiwa katika maghala.


Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Bwana Milton Lupa katika picha ya pamoja na Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Uuzaji nafaka ya Nchini Zimbabwe Bwn Rockie Mutenha baada ya utiaji saini ya mkataba wa mauzo ya mahidi