Kanda ya Shinyanga

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Shinyanga yapanga kununua Mtama kiasi cha tani 4,500

Wakala wa Taifa Kanda ya Shinyanga imepanga kununua shehena ya mtama kiasi cha tani 4,500 katika ghala lake lililopo katika Wilaya ya Serengeti katika awamu ya pili ya ununuzi itakapoanza.

Meneja wa Kanda ya Shinyanga Bibi. Mary Shangali amesema mpango huo umepangwa kutekeleza katika kipindi cha awamu ya pili ya ununuzi itakapoanza.

Bibi Shangali ameongeza kuwa mtama ni zao ambalo linalimwa kwa wingi katika Mkoa wa Mara na hususan katika Wilaya ya Serengeti na kuongeza kuwa Wakala imefikiria kununua zao hilo kwa kuwa wakazi wa Mkoa huo wanauthamini mtama zaidi kuliko mahindi kama ilivyozoeleka katika maeneo mengine.

“Zao la mtama linapatikana kwa wingi na ziada ni ya kutosha, matumizi yake ni kama mahindi. Wakazi wa maeneo ya Mkoa wa Mara wanauthamini mtama zaidi kuliko mahindi na wanatengeneza ugali na vyakula vyengine”. Amekaririwa Bibi Shangali.

Bibi Shangali aliongeza kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Shinyanga imekuwa ikihudumia Mkoa wa Shinganya, Mwanza, Mara na Kagera na kuongeza kuwa hivi karibuni Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba aliagiza Wakala kutoa kiasi cha tani 20 za mahindi kwa ajili ya familia chache za wakazi wa Wilaya ya Kyelwa na Karagwe ambao walikabiliwa na uhaba wa chakula na kwamba baada ya agizo hilo, chakula kilifika kwa walengwa baada ya siku mbili.

Bibi. Shangali aliongeza kuwa mwezi mmoja baada ya kutolewa kwa chakula hicho, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa kiliwasiliana na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Shinyanga kwa ajili ya kutoa tena chakula kiasi cha tani 200 kwa ajili ya familia zilizokumbwa na ukame katika Wilaya hizo.

“Ni kweli Ofisi ya Waziri Mkuu – Kitengo cha Maafa kiliratibu zoezi hilo na kiasi cha tani 200 kilisafirishwa mpaka katika Wilaya ya Kyelwa na Karagwe na kukabidhiwa kwa Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kwa ajili ya kugawiwa kwa familia zilizokumbwa na uhaba wa chakula, uliotokana na ukame baada ya mvua kukosekana katika kipindi cha msimu wa kilimo.” Amekaririwa Bibi. Shangali.