BEI YA UNUNUZI WA AKIBA YA CHAKULA YA TAIFA MSIMU WA 2021/2022

TANGAZO KWA UMMA

BEI YA UNUNUZI WA AKIBA YA CHAKULA YA TAIFA MSIMU WA 2021/2022

Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hununua nafaka kila mwaka kwa ajili ya akiba ya chakula ya Taifa. Wakala umeanza rasmi ununuzi kwa msimu wa 2021/2022 tarehe 15 Agosti, 2021. Kwa kuanzia, Wakala umefungua vituo vya ununuzi wa mahindi kwenye kanda zenye uzalishaji mkubwa wa mahindi zinazojumuisha Mikoa ya Songea, Njombe, Songwe, Mbeya, Rukwa na Katavi.

Kutokana na maelekezo ya Serikali, Wizara ya Kilimo kupitia Wakala unanunua mahindi kwa bei ya shilingi 500 kwa kilo katika vituo vikuu vya Wakala (vituo vyenye ghala kuu za Wakala).

Aidha, bei ya kununulia mahindi katika vituo ambavyo vipo nje ya vituo vikuu itakuwa chini ya shilingi 500 kwa kilo, ambapo Wakala kupitia kanda zinazonunua mahindi utabainisha bei ya halisi itakayotumika katika vituo husika. Bei hizo zitapangwa kwa kuzingatia umbali kati ya vituo vidogo na vituo vikuu na miundombinu mingine ya usafirishaji wa shehena ya nafaka inayonunuliwa katika vituo vidogo kwenda vituo vikuu.

  • Imetolewa na:
  • Afisa Mtendaji Mkuu
  • Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)