Kanda ya Dodoma

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Dodoma imefanikiwa kununua tani 8,692 za mahindi katika msimu wa kilimo wa 2016/2017

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Dodoma imefanikiwa kununua shehena ya mahindi kiasi cha tani 8,692 katika msimu wa ununuzi wa 2016/2017.

Akiongea katika mahojiano maalum, Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi Chakula, Kanda ya Dodoma, Bwana Ramadhan Mkilindi amesema Wakala ilifanikiwa kununua kiasi hicho cha mahindi licha ya msimu huu kuwa na ziada kidogo katika maeneo kadhaa ya Mkoa wa Dodoma na Singida.

Bwana Mkilindi aliongeza kuwa katika Mkoa wa Dodoma pekee, Wakala ilifanikiwa kununua kiasi cha tani 5,692 za shehena ya mahindi ambapo Kata ya Kizota pekee, iliongoza kwa kuiuzia Wakala kiasi cha tani 1,500.

Meneja wa Kanda ya Dodoma Bwana Mkilindi ameongeza kuwa Kituo cha Manyoni kimefanikiwa kununua shehena ya mahindi kiasi cha tani 3,000 na kiwezesha Kanda kuwa imenunua kiasi cha tani 8,692 huku lengo ambalo Wakala Kanda hiyo ilikuwa imejiwekea kununua tani 10,000.

Bwana Mkilindi aliongeza kuwa Kanda ya Dodoma imekuwa ikipokea chakula hususan mahindi kuliko kununua, hali hiyo inatokana na sababu za Kijiografia ya kuwa Kanda ya kati yenye Mkoa wa Dodoma na Singida imekuwa ikipata mvua za chini ya wastani kila mwaka.

"Kimsingi Kanda yetu uwa inapokea kwa sehemu kubwa kuliko kununua, hii inatokana na asili ya eneo la Mkoa Dodoma na Singida na kama unavyofaham majukumu ya Wakala ni kununua, kuhifadhi na kutoa au kuhamisha chakula kutoka Kanda moja kwenda nyingine, wakati wa uhitaji". Amekaririwa Bwana Mkilindi.

"Na kwa sababu Wakala ununua chakula kutoka maeneo yenye uzalishaji mkubwa na ziada ya kutosha, ndiyo maana tumenunua kidogo kwa Dodoma na Singida lakini pia tumeona tuanze kununua pia katika Mkoa wa Manyara ambapo kuna ziada ya kutosha" Ameongeza Bwana Mkilindi.

Bwana Mkilindi aliongeza kuwa uwezo wa kuhifadhi katika Kanda ya Dodoma ni tani elfu 34,500, Dodoma Mjini ni tani elfu 30,000 na Manyoni Mkoani Singida ni tani 4,500.

Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (World Food Program - WFP) latoa msaada wa mashine ya kusafisha mahindi kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Dodoma

Meneja wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula Kanda ya Dodoma Bwana Ramadhan Mkilindi amesema Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (World Food Program) limetoa msaada wa mashine ya kusafishia mahindi na kwa lengo la kuongeza ubora wa bidhaa hiyo na kuongeza ufanisi na kurahisiha kazi ya kuyaanda mahindi wakati wa msimu wa ununuzi.

Akiongea katika mahojiano maalum, Bwana Mkilindi amesema kwa kipindi kirefu Shirika la WFP limekuwa mdau na mbia wa maendeleo kwa kushirikiana na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na kuongeza kuwa mashine hiyo itaongeza tija katika kuongeza thamani ya mahindi ya Wakala Kanda ya Dodoma, ambayo yamekuwa yakiuzwa kwa Taasisi hiyo.

Akizungumzia kuhusu ubora na uwezo wa mashine hiyo, Mthibiti wa Ubora wa Kanda ya Dodoma Bwana Felix Ndunguru anasema mashine hiyo ni ya kisasa na ina uwezo wa kusafisha mahindi kiasi cha tani 80 kwa saa na kwamba itaongeza ufanisi kwa kiwango kikubwa wakati itakapoanza kutumika katika msimu ujao wa ununuzi.

"Mashine ni ya kisasa na itaongeza ufanisi kwa kuwa inasafisha, tani 80 kwa saa, kiwango hicho ni kikubwa, tunatarajia mabadiriko makubwa wakati wa kuanza kuitumia wakati wa msimu mpya wa ununuzi na kwa sehemu kubwa itapunguza idadi ya vibarua walikuwa wakifanya kazi ya kusafisha mahindi kwa njia za kawaida". Alikaririwa Bwana Nduguru.

Bwana Ndunguru amekaririwa "Tumepewa mashine hii kutoka kwa WFP na wamesema wameitoa kwa sababu, wamekuwa wakinunua mahindi mengi kutoka kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kila mwaka".

Akifafanua kuhusu mashine hiyo kutoka kwa WFP, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara Bwana Joseph Ogonga amesema, msaada huo wa mashine hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano (MoU) katika ya Taasisi hiyo na Wakala na kwamba kumekuwa na mahusiano ya muda mrefu ya kikazi na kibiashara na kuongeza kuwa kiasi cha fedha za kununulia mashine hiyo, hazijawekwa wazi na Shirika la WFP.