Kanda ya Arusha


MHE MWANJELWA ATEMBELEA WAKALA WA TAIFA WA HIFADHI YA CHAKULA (NFRA)-ARUSHA

Naibu waziri wa Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa leo Octoba 29, 2017 ametembelea Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula zilizopo Mtaa wa Njiro Mkoani Arusha ili kujionea namna wanavyofanya kazi kutekeleza majukumu yao.

Mhe Mwanjelwa ametembelea Ofisi hizo ambapo pamoja na mambo mengine amekagua maghala yanayotumika kuhifadhi chakula ambapo amejionea ukubwa wa maghala hayo na jinsi kanda ya Arusha ilivyo na uwezo wa kuhifadhi chakula wastani wa Tani 39000.

Pia alijionea akiba kubwa iliyopo ghalani ya mahindi katika msimu huu wa mwaka 2017/2018 ambayo ni Jumla ya tani 3,997.664 ambazo hizo ni pamoja na salio la mahindi la msimu uliopita 2016/2017 ambazo zilikuwa Tani 2,997.664

Akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa NFRA Mhe Mwanjelwa aliwapongeza kwa uwajibikaji huku akiwasihi kuongeza ufanisi na ubunifu katika kutekeleza majukumu yao ikiwa ni pamoja na kuzikabili changamoto mbalimbali ikiwemo ile ya ufinyu wa bajeti.

Mhe Mwanjelwa alisema kuwa sifa ya mtumishi mzuri ni yule mwenye uwezo wa kukabiliana na changamoto ili kutimiza adhma ya serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli katika kukuza ufanisi katika kazi kwa kutimiza vyema wajibu kwa kuwa wabunifu.

Alisema kuwa watumishi wanapaswa kuongeza ushirikiano na Ari mpya ya kazi kwa kufanya kazi kwa weledi kuachana na kufanya kazi kwa mazoea.

Chimbuko la Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula lilitokana na lililokuwa shirika la Usagishaji la Taifa (NMC) mwaka 1990 ambapo dhumuni kubwa ilikuwa ni kuwepo na kitengo maalumu cha kununua, kuhifadhi, kuhudumia chakula Sehemu zenye upungufu wa chakula na kulinda bei ya soko la mahindi kwa mlaji mbali na shughuli zilizokuwa zikifanywa na NMC.

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula ipo chini ya Wizara ya kilimo na Msimamizi Mkuu wa shughuli zote za Wakala ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala (CEO).