Wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) wakiongozwa na Kaimu Mwenyekiti Bi Chabu Mwisharo, Katibu CPA . Milton Lupa na Wajumbe wa Bodi hiyo Bw. Tumaini Mbano, Bw. Benson Meitinyiku na Wakili Msomi Obadia Kameya, wamekutana na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Francis Michael na kufanya mazungumzo katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, kabla ya kuendelea na ziara yao Mkoani humo.
Dkt Francis alifurahishwa na ziara ya Bodi katika Mkoa wa Songwe iliyofanyika kwa lengo la kufuatilia mwenendo wa ununuzi wa nafaka kutoka kwa Wakulima unaofanyika kupitia NFRA.
Bodi ilieleza kwamba katika Mkoa wa Songwe maeneo mengi Wakulima wamesha vuna mazao yao hivyo waliona ni vyema Bodi ikatembelea maeneo hayo kujionea kasi ya upatikanaji wa nafaka hizo na kuangalia namna watakavyoweza kuboresha zoezi hilo ili kuwarahisishia Wakulima.
"Nazani mmepita maeneo mengi wakati mnaingia Songwe na kujionea wakulima wakiwa wameanika mazao yao nje, hii ni ishara kwamba mazao yapo na nawahikikishia sisi kama Mkoa tutashirikiana na nyie kwa lolote lile". amesema Dkt Francis.