Habari

MAAFISA TOKA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR WAFANYA ZIARA YA KIKAZI NFRA MAKAO MAKUU

MAAFISA TOKA SERIKALI YA MAPINDUZI YA ZANZIBAR WAFANYA ZIARA YA KIKAZI NFRA MAKAO MAKUU
Oct, 02 2023

Ujumbe kutoka Wizara ya Kilimo Umwagiliaji Maliasili na Mifugo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wamefanya ziara ya kutembelea Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA). Ujumbe huo uliwajumuisha Maafisa wa tatu akiwemo Zainabu Moyo, Ally Basha na Mhandisi Salmin Hassan Ally.

Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kubadilishana uzoefu katika masuala ya Uhifadhi na utekelezaji wa majukumu ya Wakala kwa ujumla. Katika ziara hiyo Ujumbe huo ulipata fursa ya kutembelea Makao Makuu ya NFRA ambapo walifahamishwa kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wakala kwa ujumla na mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji huo.

Wajumbe hao pia walitembelea kanda ya Dodoma, ambapo waliweza kuona namna Wakala unavyohifadhi nafaka katika maghala kwa ubora wa hali ya juu na kisha kutembelea eneo la Mradi wa Kuongeza Uwezo wa Kuhifadhi Nafaka (Ujenzi wa Vihenge na Maghala ya Kisasa) unaotekelezwa katika kanda ya Dodoma na Maeneo mengine saba nchini.

Aidha, Wajumbe hao walitembelea kanda ya Arusha, Mkoa wa Manyara, katika Mji wa Babati ambapo walishuhudia namna Mradi wa Vihenge na Maghala ya Kisasa ambao umekamilika unavyofanya kazi katika eneo la Makatanini-Babati.

Ujumbe huo uliongozana na baadhi ya Viongozi kutoka NFRA akiwemo Mkurugenzi wa Masoko Bw. Mikalu Mapunda, Mkurugenzi wa Uhifadhi Dkt Silvano Mwakinyali na Meneja wa Uwekeza na Usimamizi wa Milki Mhandisi Imani Nzobonaliba.