Habari

BALOZI WA NAMIBIA AFURAHISHWA NA JUHUDI ZA TANZANIA KATIKA UHIFADHI WA CHAKULA

BALOZI WA NAMIBIA AFURAHISHWA NA JUHUDI ZA TANZANIA KATIKA UHIFADHI WA CHAKULA
Jul, 07 2023

Balozi wa Namibia Nchini , Mhe. Lebbius Tobias amefurahishwa na ufanisi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) hususani katika zoezi la uhifadhi wa Chakula kwa Taifa na namna inavyotekeleza majukumu ya kuhakikisha usalama wa chakula nchini.

Mhe. Balozi amesema hayo alipotembelea Banda la NFRA katika Maonesho ya 47 ya *Kimataifa* ya Biashara 77 jijini Dar Es Salaam, ambapo alipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Masoko wa NFRA Bw. Mikalu Mapunda, kuhusu majukumu ya NFRA na utelelezaji wake katika kuchangia usalama wa chakula nchini.

Mhe. Balozi alielezwa kuhusu dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuifanya NFRA kuwa kitovu cha chakula kwa nchi za ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini, na jinsi Serikali kupitia NFRA ilivyoweza kusaidia nchi jirani katika upatikanaji wa chakula kwa vipindi mbalimbali.

Aidha, Mhe. Balozi Lebbius Tobias alivutiwa na maendeleo yaliyofikiwa na Wizara ya Kilimo kupitia Wakala kwa kuanza kutumia miundombinu ya kisasa katika uhifadhi.

Mhe. Balozi amepongeza sana juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha Nchi inakuwa na usalama wa Chakula na hata kusaidia Nchi za jirani.

" Nimefurahishwa sana kuona Taifa la Tanzania linapambana vilivyo kwenye uhifadhi wa Chakula, kwa ziara hii nimeweza kubaini kwamba hata Namibia ikiwa na upungufu wa chakula tuna sehemu ya kukimbilia” amesema Mhe. Balozi Lebbius Tobias.