Habari

RC OLE SENDEKE AIOMBA (NFRA) KUTENGENEZA SOKO LA WAKULIMA NJE YA NCHI

RC OLE SENDEKE AIOMBA (NFRA) KUTENGENEZA SOKO LA WAKULIMA NJE YA NCHI
Apr, 25 2018

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umetakiwa kuwasaidia wakulima nchini kutengeneza soko la mazao mbalimbali wanayozalisha hususani mahindi ili kupata soko la kuridhisha nje ya nchi.

Jukumu hilo endapo kama NFRA italifanya la kutafuta na kuboresha masoko ya mazao nje ya nchi linatazamiwa Kuimarisha soko na kuchangamsha bei jambo ambalo litawanufaisha wakulima kote nchini hivyo kuona umuhimu wa nguvu kazi wanazotumia katika kilimo.

Mwito huo ulitolewa hivi karibuni na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe Christopher Ole Sendeka wakati akizungumza na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) Bi Vumilia L. Zikankuba Ofisini kwake Mkoani Njombe.

Katika kuimarisha uhifadhi mahususi wa maeneo ya kuhifadhia chakula tayari NFRA imezindua ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa ambapo katika Halmashauri ya Mji wa Makambako Mkoani Njombe vitajengwa Vihenge vyenye uwezo wa kuhifadhi Tani 20,000 sambamba na Tani 20,000 za maghala hivyo kufanya uwezo wa kuhifadhi kuwa tani 79,000 kutoka uwezo wa sasa wa Tani 39,000.

Sambamba na hayo pia Mhe Ole Sendeka amewaomba wananchi kote nchini kuanzisha utamaduni mahususi wa kununua chakula na kuhifadhi kwani kufanya hivyo itatoa urahisi wa kuuzwa kwa ziada inayosalia.

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unamiliki maghala ya kuhifadhi nafaka 34 kote nchini yenye uwezo wa jumla ya Tani 251,000.

Aidha, Uwezo huu wa sasa wa maghala hautoshelezi mahitaji ya dharula ya chakula kwa mfululizo wa miezi mitatu kwa akiba isiyo pungua Tani 700,000, hivyo kupelekea uhitaji wa kuongeza uwezo wa uhifadhi. Hivyo, mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa ambao ulizinduliwa juzi 21 Aprili 2018 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa (Mb), umeanzishwa ili kukidhi lengo la Wakala kuhifadhi chakula kisichopungua Tani 700,000.

Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula (NFRA) Bi Vumilia L. Zikankuba alimuhakikishia Mkuu huyo wa Mkoa wa Njombe kuwa Wakala umejipanga vyema kutekeleza majukumu yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa serikali inakuwa na akiba ya kutosha ya mazao ili kukidhi matakwa ya majukumu ya msingi ya kuwahudumia wananchi kwa mujibu wa dira ya kuwa taasisi yenye uwezo wa kukabiliana na upungufu wa chakula kwa wakati ifikapo mwaka 2020.