Habari

MAAFISA UGANI NCHINI WATAKIWA KUWA NA MASHAMBA YA MFANO

MAAFISA UGANI NCHINI WATAKIWA KUWA NA MASHAMBA YA MFANO
Jul, 18 2018

Agizo hilo limetolewa jana 17 Julai 2018 na Naibu waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula akiwa katika ziara ya kikazi ya kutembelea taasisi za umma ili kujionea namna ya uendeshaji na utendaji wa taasisi hizo.

“Tumekuwa na maafisa ugani kila kona nchini lakini hawana hata heka moja ya mashamba, sasa tunategemea wakulima wetu wajifunze vipi kupitia wataalamu wetu ambao tumewaajiri, hivyo ili kuwa na tija katika uzalishaji wa mazao kwa kutumia mbinu bora za kilimo cha kisasa ni lazima maafisa ugani kuwa na maeneo ya kulima ambayo yatatumika kama mashamba darasa” Alikaririwa Mhe Mgumba

Alisema pamoja na kuwepo kwa wataalamu hao wa kilimo bado uzalishaji wa mazao mbalimbali nchini yakiwemo mazao ya chakula na biashara si wa kuridhisha ambapo wakulima wanalima na kupanda pasina hata kufuata hatua za kitaalamu.

Mhe Mgumba aliongeza kuwa lengo la Serikali kusambaza Maafisa Ugani kwenye Halmashauri mbali mbali nchini ilikuwa kuwasaidia wakulima waweze kufanya Kilimo kwa Ufanisi na kuongeza mavuno lakini imekuwa kinyume maafisa ugani wanajifungia ofisini badala ya kwenda shambani walipo wakulima.

Naibu Waziri huyo wa kilimo amepongeza mradi wa ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa huku akisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli inaendelea na utekelezaji wa mkakati wa kuwanufaisha wakulima kupitia kilimo sambamba na kuimarisha bei ya mazao yao.

Alisema Serikali imefungua mipaka na inaendelea na jitihada za kutafuta masoko ya nje pamoja na kuboresha miundombinu ya kuhifadhi chakula kwa kujenga maghala na vihenge vya kisasa katika maeneo mengine yenye uzalishaji mkubwa wa chakula.

Akitoa taarifa ya mradi huo wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi,Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya chakula Bi Vumilia L. Zikankuba alisema kuwa mradi huo pindi utakapokamilika utafungua fursa kubwa kwa wakulima nchinikwani uwezo wa kuhifadhi wa Wakala wa Taifa wa Kuhifadhi Chakula utakuwa mara mbili ya uwezo wa sasa yaani kutoka tani 251,000 hadi tani 501,000 huku ikitarajiwa kufikia Tani 700,000 kufikia mwaka 2025.

Bi Vumilia alieleza kuwa Mikataba ya mradi wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula, ilisainiwa na kuanza kazi tarehe 09 Desemba 2017 kati ya (NFRA) na makampuni mawili toka nchini Poland ambayo ni Feerum S.A na Unia Araj Realizacje Sp.o.o. Aidha, mradi huo utatekelezwa kwa gharama ya Dola za kimarekani milioni 55 na unatarajiwa kukamilika ndani ya kipindi cha miezi kumi na nane (18) kuanzia mwezi Mei 2018.

Bi Zikankuba, aliongeza kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula unamiliki maghala ya kuhifadhi nafaka 34 yenye uwezo wa jumla ya Tani 251,000. Uwezo huu wa sasa wa maghala hautoshelezi mahitaji ya dharula ya chakula kwa mfululizo wa miezi mitatu kwa akiba isiyo pungua Tani 700,000, hivyo kupelekea uhitaji wa kuongeza uwezo wa uhifadhi.

Kwa picha zaidi tembelea: https://wazo-huru.blogspot.com/2018/07/maafisa-ugani-nchini-watakiwa-kuwa-na.html