Habari

WAZIRI WA KILIMO MHE JAPHET HASUNGA AZINDUA MTAMBO WA KUSAFISHA NAFAKA KWA NFRA ULIOTOLEWA NA WFP

WAZIRI WA KILIMO MHE JAPHET HASUNGA AZINDUA MTAMBO WA KUSAFISHA NAFAKA KWA NFRA ULIOTOLEWA NA WFP
Mar, 17 2019

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) amezindua mtambo wa kusafisha nafaka kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) uliokabidhiwa na Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

Akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano ya mtambo huo Waziri Hasunga ameishukuru WFP kwa tukio hilo ambalo linadhihirisha ushirikiano wa karibu uliopo kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mpango wa Chakula Duniani.

Alisema WFP imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo nchini kwa muda mrefu na kwa upande wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, ushirikiano huo umedumu tangu mwaka 2012 ambapo WFP na NFRA wamekuwa wakishirikiana kikamilifu katika kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya pande zote mbili.

“Mpango Mkakati wa WFP wa miaka mitano (Country Strategy Plan 2017-2021) unaendana na mipango ya Serikali inayolenga kufikia Maendeleo Endelevu ya Dunia (SDGs), hususani lengo la kutokomeza njaa (zero hunger) ifikapo mwaka 2030” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa

“Mfano, mkakati wa WFP wa kuwasaidia wakulima wadogo kupitia mpango wa Farm to Market Alliance (FTMA) unashabihiana na Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini (ASDP II), kwa kuwa mikakati yote imelenga katika kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji, kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno, kuongeza thamani ya mazao na kufikia masoko”

Alisema, kutokana na mkakati huo, Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli, inathamini na kuipongeza WFP katika kuimarisha usalama wa chakula na lishe hapa nchini.

Aidha, Serikali inaishukuru WFP kwa kuichagua Tanzania kuwa moja wapo ya Kituo cha Usimamizi wa Bidhaa za Kimataifa (Global Commodity Managed Facility) ambacho kinasaidia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa masoko ya mazao ya chakula kwa wakulima nchini.

Aliongeza kuwa mtambo huo ambao umekabidhiwa kwa Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula (NFRA) wenye thamani ya Dola za Kimarekani Laki 170.841 (Laki moja na sabini nukta nane nne moja) sawa na Shilingi za Kitanzania milioni 399.8 (milioni mia tatu tisini na tisa nukta nane) ni udhibitisho wa nia njema ya WFP kushiriki katika jitihada za Serikali ya awamu ya tano kuifanya Tanzania kuwa yenye uchumi wa viwanda.

Mtambo huo una uwezo wa kusafisha mahindi zaidi ya tani 100 kwa siku. Ni dhahiri kuwa mtambo huo utaboresha utendaji na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa shughuli za NFRA.

Aidha, Mhe Hasunga aliitaka Menejimenti ya NFRA, kuhakikisha kwamba mtambo huo unatunzwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa huku akiiomba WFP kuangalia uwezekano wa kuisaidia NFRA mitambo ya namna hiyo ya kuhamishika (Mobile Grain Cleaning Machine), kwa kuwa sehemu kubwa ya ununuzi wa mahindi hufanyika katika vituo vya ununuzi vijijini.

Alitumia nafasi hiyo pia kuishukuru kwa mara nyingine WFP kwa kununua tani 36,000 za mahindi kutoka NFRA na kuiomba iongeze kiwango cha nafaka kinachonunuliwa nchini kwa ajili ya shughuli zao kupitia sekta binafsi na taasisi za Serikali ikwemo NFRA na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB).