Habari

Rais Magufuli aipongeza NFRA kuingia mkataba wa Tani 36,000 wa mauziano ya mahindi na WFP

Rais Magufuli aipongeza NFRA kuingia mkataba wa Tani 36,000 wa mauziano ya mahindi na WFP
Jan, 05 2019

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli Leo tarehe 4 Januari 2019 ameshuhudia utiaji saini mkataba wa mauziano ya mahindi kati ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la chakula Duniani (WFP).


Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika Ikulu Jijini Dar es salaam Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya kilimo kwa kuwatafutia masoko wakulima na kuongeza kuwa inapaswa kuongeza msisitizo wa kutafuta masoko ya Mazao mengine ya wakulima nchini.


Pamoja na pongezi hizo za Mhe Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya kilimo kupitia NFRA na kuiagiza Wizara ya kilimo kushirikiana na Taasisi zingine za serikali ikiwemo jeshi la Polisi, Wakala wa Barabara (TANROADS), Shirika la viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Shirika la reli Tanzania (TRC), na mamlaka ya usimamizi wa bandari (TPA) kuhakikisha wanaondoa urasimu na kuharakisha ununuzi wa Mazao yanayonunuliwa na WFP ikiwemo Tani 36,000 za mahindi ili wakulima wanufaike na fursa hiyo.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya mawasiliano ya Rais Ikulu imeeleza kuwa mkataba huo umetiwa saini na Kaimu Mtendaji Mkuu wa NFRA Bi Vumilia Zikankuba na Mwakilishi wa Mkurugenzi mkazi wa WFP hapa nchini Bw Michael Danford ambapo WFP inanunua mahindi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 21 kutoka NFRA.


Mhe Rais Magufuli ameipongeza WFP kwa uamuzi wake wa kununua chakula kutoka Tanzania kwa ajili ya kusaidia wakimbizi wa nchi zenye matatizo ya chakula na ameitaka NFRA kutoa Tani zote 45,000 za mahindi ambazo WFP waliomba kununua, ili fedha hizo zitakazopatikana ziweze kununua mahindi mengine kwa wakulima.


Vilevile Rais Magufuli ameiagiza NFRA kuuza mahindi kwa WFP hata kama watahitaji mahindi Tani 100,000 au 200,000 kwani kufanya hivyo kutawarahisishia kwenda sokoni kununua mahindi mengine jambo ambalo linaimarisha soko la wakulima.


Ameitaka NFRA kujipanga vizuri ili kujiendesha kwani serikali haitotoa fedha kila mwaka kwa ajili ya kununua mahindi ya kuhifadhi huku akiwataka wafanyabiashara kuacha kulalamika badala yake kufanya biashara kwa uwazi na serikali itawaunga mkono.


Awali, Naibu Waziri wa kilimo Mhe Innocent Bashungwa alisema kuwa Wizara ya kilimo imejipanga kuimarisha soko la wakulima ndani na nje ya nchi hivyo wakulima hawapaswi kuwa na wasiwasi badala yake wanapaswa kuongeza tija katika uzalishaji kwani serikali knawatafutia soko.


Bashungwa alisema kuwa Wizara ya kilimo imechukua hatua kadhaa za kuimarisha mazingira kwa WFP kunua mahindi na Mazao mengine hapa nchini ambapo jambo hilo litafanyika sambamba na kufungamanisha uchumi wa Viwanda.


MWISHO.