Habari

NFRA LAZIMA INUNUE MAZAO YA KUTOSHA KWA WAKULIMA

NFRA LAZIMA INUNUE MAZAO YA KUTOSHA KWA WAKULIMA
Mar, 10 2019

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umetakiwa kununua mahindi mengi kwa wakulima kwani kufanya hivyo kutaongeza wigo wa masoko kwa wakulima wa mazao mbalimbali ya nafaka nchini.

Mbunge wa Jimbo la Vwawa Mkoani Songwe ambaye pia ni Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji na kata ya Wasa vilevile katika kijiji cha Ibebwa kilichopo katika kata ya Msia akiwa katika ziara jimboni humo kukagua utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwenye miradi ya maendeleo.

Mhe Hasunga alisema kuwa NFRA inapaswa kubadili dhana ya kununua mahindi kwa ajili ya hifadhi pekee badala yake wanapaswa kununua mahindi kwa ajili ya kuyauza ili kuongeza ufanisi wa soko kwa wakulima nchini.

Katika hatua nyingine alisema kuwa tayari NFRA imeanza kutekeleza maelekezo ya serikali kwa kununua na kuuza mahindi kupitia mkataba na Mpango wa Chakula Duniani (WFP) utakaopelekea kurejea sokoni kununua mahindi kwa wakulima.

Alisema NFRA pamoja na Bodi ya Nafaka na Mazao mchanganyiko zinapaswa kutekeleza wajibu wake katika ufanyaji biashara ya mazao.