Habari

NAIBU WAZIRI WA MADINI ATOA HEKO KWA NFRA KWA ELIMU WANAYOITOA KUHUSU UHIFADHI WA MAHINDI BAADA YA KUVUNA

NAIBU WAZIRI WA MADINI ATOA HEKO KWA NFRA KWA ELIMU WANAYOITOA KUHUSU UHIFADHI WA MAHINDI BAADA YA KUVUNA
Sep, 11 2018

Naibu Waziri wa Madini Mhe Stanslaus Nyongo amepongeza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula nchini (NFRA) kwa elimu wanayoitoa kuhusu njia bora za kuhifadhi nafaka ya mahindi mara baada ya kuvuna.

Nyongo ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na uongozi wa NFRA mara baada ya kutembelea banda la NFRA kwenye maadhimisho ya maonesho ya kilimo na sherehe za wakulima Nanenane Kitaifa yaliyofanyika katika Viwanja vya Nanenane Halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu ambapo Rais mstaafu wa srikali ya awamu ya tatu Mhe Benjamini Willium Mkapa ndiye alikuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho hayo.

Pamoja na mambo mengine Mhe Naibu Waziri Nyongo amepongeza elimu inayotolewa kuhusu utunzaji huo wa mahindi mara baada ya kuvuna kwa kufuata taratibu zote za kuvuna wakati muafaka, ikiwa ni pamoja na Kukausha vizuri mahindi baada ya kuvuna.

Mhe Nyongo pia amepongeza elimu inayotolewa na NFRA kuhusu utambuzi wa mahindi kama yamekauka kwa kutumia njia za kienyeji ambazo ni rafiki kwa wakulima wa chini pamoja na njia za kisasa.

Pia alijionea na elimu kuhusu matumizi bora ya mifuko ya kuhifadhia mahindi ikiwa ni pamoja na mifuko ya PICS, Vihenge vya chuma sambamba na maghala ya tofali.

Alisema kuwa njia hizo zitaleta ufanisi iwapo mahindi yameandaliwa vizuri kabla ya kuhifadhi huku akiisihi NFRA kuongeza nguvu katika utoaji elimu ili wakulima waweze kunufaika kwani mkulima akielimika ipasavyo ni sehemu ya mafanikio ya mtu mmoja mmoja sambamba naukuzaji wa uchumi wa Taifa.