Habari

KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO MHANDISI MTIGUMWE AIAGIZA NFRA KUNUNUA MAHINDI

KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO MHANDISI MTIGUMWE AIAGIZA NFRA KUNUNUA MAHINDI
Jan, 08 2019

Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe, leo tarehe 07 Januari 2019, ameuagiza uongozi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuendelea kununua mahindi ya wakulima kwa bei ya sh. 450 kwa kilo.

Mhandisi Mtigumwe ametoa agizo hilo wakati akizungumza kwenye kikao kazi na Maafisa Kilimo wa Wilaya za Mkoa Wa Katavi, Wadau mbalimbali wa Kilimo wakiwemo mawakala wa pembejeo, wasindikaji, wawakilishi wa vyama vya msingi vya ushirika na wakulima, kilichofanyika katika ukumbi wa Polisi Wilayani Mpanda mkoa wa Katavi.

Katibu Mkuu huyo ameitaka NFRA kununua mahindi kwa wakulima kwani kufanya hivyo kutaimarisha soko la wakulima Wa mahindi nchini ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Wizara ya Kilimo sambamba na agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli la kutafuta masoko ya Mazao ya wakulima.

Alisema kuwa Wizara ya Kilimo imeanza mkakati rasmi wa kutafuta masoko ya Mazao mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kuanzisha kikosi maalumu kitakachoshughulikia dhamira hiyo.

Akiwa katika ziara hiyo mkoani Katavi, Katibu Mkuu ametembelea maduka ya mawakala wa pembejeo za kilimo na kujionea hali ya upatikanaji wa pembejeo za mbegu na mbolea mkoani Katavi.

Alisema kuwa pembejeo za kilimo zikiwemo mbolea ni nyenzo muhimu kwa mkulima katika kipindi hiki cha msimu wa kilimo.

Pia, ametembelea maghala ya wafanyabiashara wa mbolea, kiwanda cha kusindika mahindi, mpunga na alizeti.

Katika hatua nyingine katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe amesema kuwa Wizara ya Kilimo ipo katika mapitio ya sifa za Viongozi wa vyama vya ushirika nchini ili kupata viongozi watakao ongoza kwa weledi sekta ya Ushirika nchini.

Alieleza kuwa zipo nafasi za uongozi katika vyama vya ushirika ambazo zinahitaji utaalamu na si tu kuchagua kiongozi anayejua kusoma na kuandika, mfano Mhasibu.

Alisema, dhana ya kuchagua viongozi wa Ushirika wenye sifa ya kujua kusoma na kuandika imeanza kupitwa na wakati hivyo yanahitajika mabadiliko jadidu katika sekta hiyo.

MWISHO.