Wakala Wa Taifa Wa Hifadhi Ya Chakula

Matukio

29 May 2016

Maafisa ubora na watunza stoo watashiriki mafunzo ya kuwaweka tayari kwaajiri ya msimu unaokuja wa ununuzi wa chakula.

Wakala wa Taifa Hifadhi ya Chakula yatimiza agizo la Waziri wa Kilimo ndani ya Saa 72

Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Kanda ya Shinyanga jana ilitimiza agizo la Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Mhe. Dkt. Charles Tizeba, agizo la kuupa Mkoa wa Kagera kiasi cha mahindi tani 20 ili kusaidia Kaya kadhaa zinazokabiliwa na upungufu wa chakula mkoani humo.

Akikabidhi Msaada huo kwa niaba ya Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula, Kaimu Mkurugenzi wa Mipango na Uendeshaji, Bwana Nicodemus Masao alisema, Wakala imetekeleza agizo la Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi kama alivyoagizwa ya kwamba msaada huo ni dharura, ufike kwa walengwa, haraka iwezekanavyo.

“Nakabidhi msaada huu, mahindi kiasi cha tani 20 kama Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi alivyoagiza, na naomba uende kwa walengwa sawa sawa uhitaji” Alikaririwa Bwana Masao.

Akipokea msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenelali Mstaafu, Salum Kijuu alisema, Mkoa unaishukuru Serikali Kuu kwa msaada huo wa haraka na aliahidi kuwa utaenda kwa walengwa kama tathmini zinavyoonyesha.

“Napenda nimuhakikishe Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi kuwa, msaada huu wa mahindi kiasi cha tani 20, utawafikia walengwa, sambamba na tathmini yetu kwa Kaya zenye upungufu” Alikaririwa Mkuu huyo wa Mkoa.

Itakumbukwa kuwa katika Siku ya Maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani ambayo Kitaifa iliadhimishwa bila shamrashamra katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Waziri wa Kilimo Mifugo na Uvuvi, Dkt. Tizeba alisema siku moja kabla ya maadhimisho hayo, yaani, tarehe 15/10/2016 alipata nafasi ya kutembelea Halmashauri mbili ambapo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa na Misenyi alijionea namna ambavyo ukame umeathiri uzalishaji wa mazao ya chakula kama ndizi.

Aidha, katika Wilaya Kyerwa aliitembelea familia moja, ambayo wazazi walitelekeza watoto wao kwa sababu ya hali ya ukame iliyosababisha Kaya kadhaa kukumbwa na uhaba wa chakula na baadae alielekea Wilaya ya Misenyi nako hali ilikuwa hivyo hivyo na baada ya kumaliza ziara yake hiyo, Dkt. Tizeba aliiagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula kuhakikisha inaleta mahindi kiasi cha tani 20 ili chakula hicho, kigawanywe kwenye Kaya zilikabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula.

Katika maadhimisho hayo yaliyokuwa na kaulimbiu iliyosema: ‘‘Mbinu za Uzalishaji wa Chakula ziendane na Mabadiliko ya Tabianchi’’. Dkt. Charles Tizeba alisema kauli mbiu hii, imechaguliwa kwa wakati na kwamba sasa ni itekelezwe kwa vitendo.

Waziri Tizeba alisema, athari za mabadiriko ya tabianchi dunia zinaonekana kila mahali na mfano ni mkoani Kagera na kuongeza Wakulima na Wafugaji wafikirie kubadirika kulingana na mazingira yanavyobadirika.

“Ndugu zangu wa Kagera, kama wewe ni mkulima lima mazao yanayostahimili ukame na yanayokomaa katika kipindi kifupi na tuanze kubadirika hata kimtazamo, yale mambo ya kuamini chakula kimoja ndiyo chakula pekee, tuache” Alikaririwa Waziri Tizeba.

Dkt. Tizeba alitoa mfano kuwa alipokuwa Wilayani Kyerwa aliitembelea familia moja ambayo imepoteza sehemu kubwa ya shamba la migomba na baada ya kuzunguka nyuma ya nyumba, alikuja kufahamu kuwa, Kaya hiyo ilikuwa na kihenge ambacho kilikuwa na akiba ya kutosha ya mahindi.

Waziri Tizeba aliongeza kuwa, Kaya hiyo uwezi kusema inatatizo la chakula bali mtazamo wao unawaambia kuwa chakula kikuu kwao ni ndizi pekee yake, na kusisitiza ni wakati muhafaka sasa watu wabadirike.

 

Copyright © National Food Reserve Agency 2014. All Rights Reserved